Featured

    Featured Posts

Diamond nae kwenye madawa yuma Sio Chid Benz tu, Uteja wa Madawa ya Kulevya Bongo Flava Upo Namna

Ni matunda ya saikolojia mgeuko, au unaweza
kuita saikolojia kinyumenyume (reverse
psychology). Yanayokatazwa yanavutia zaidi
watu kuyatenda. Hakuna mtu ambaye hajui
athari za matumizi ya madawa ya kulevya
lakini kuna watu huwaambii kitu.
Madawa ya kulevya ni sumu, ni kifo,
inatangazwa hivyo leo, yule aliyekuwa
anasikiliza tangazo, kesho anaanza kutumia.
Hiyo ndiyo inaitwa reverse psychology, na
mara nyingi huwasumbua sana vijana, maana
damu inachemka, nguvu ya mwili
inawadanganya.
Unadhani wakati Rehema Chalamila ‘Ray C’
anaanza kutumia ‘unga’ alikuwa hajui madhara
yake? Ni kama ambavyo Rashid Makwilo
‘Chidi Beenz’ alivyo na taarifa zote muhimu
kuhusu sumu iliyomo kwenye mihadarati lakini
hivi karibuni alikamatwa nayo Air Port.
Chidi alitangaza sana mwaka juzi kwamba
ameachana na matumizi ya madawa ya
kulevya. Binafsi niliamini kwa namna
alivyokuwa anazungumza kwenye vyombo vya
habari. Hata hivyo muonekano wake ulikuwa
unatia shaka kidogo kuamini kama kweli
kaacha.
Namfahamu Chidi, ni mwanamuziki wa Hip
Hop aliyekamilika sana. Sauti yake pekee ni
mtaji, kwani anaweza kupanda, kushuka na
kuigeuza alivyotaka, vilevile anayo staili
inayomfanya awe wa kipekee. Ni mkali wa
miondoko (swagger) ambayo inampa thamani
ya kuwa mwana-Hip Hop mwenye mvuto.
Chidi ana pumzi na nguvu (energy) akiwa
jukwaani. Kwa tathmini yangu kama
mwandishi wa habari, vilevile mdau katika
soko la muziki (hasa kizazi kipya) na sekta ya
burudani Tanzania kwa jumla, nathubutu
kusema ndiye mwanamuziki wa Hip Hop
ambaye hutumia nguvu nyingi jukwaani na
kumudu kufanya shoo kwa muda mrefu tena
kwa ufanisi.
Mara kadhaa niliwahi kujiuliza, kama alikuwa
anaonesha uwezo huo jukwaani ilhali anatumia
‘madude’, je, angekuwa hatumii? Bila shaka
angeweza kufanya zaidi. Jicho langu kimuziki
linaniaminisha kuwa Chidi alizaliwa ili awe
mwanamuziki wa Hip Hop. Ni mkali siyo siri!
Ni mmoja kati ya wanamuziki wachache wa
Hip Hop nchini wenye uwezo wa kutumbuiza
kwa ‘live band’ na kukonga nyoyo za hadhira
kwa kiwango cha juu. Kama wewe ni shabiki
wa Hip Hop, unataka nini kingine pale Chidi
anapokuwa jukwaani kifua wazi?
Nimeshafanya kazi nyingi na Chidi, pamoja na
sifa yake inayojulikana kwa wengi kwamba ni
rapa mkorofi ambaye mara kwa mara
hukwaruzana na wasanii wenzake na watu
wengine lakini upande ninaoutambua ni kuwa
mwanamuziki huyo si kigeugeu kwenye kazi.
Ni mtata sana, hilo hata yeye mwenyewe
anajijua. Kujisema kwa watu kuwa ni mkorofi
haoni tabu. Siku moja, sikumbuki tarehe ila
ilikuwa mwaka juzi, nilipokuwa namtuliza
asimvae mtangazaji wa EATV, Allan Lucky,
aliniambia yeye ni “arnimal”, akimaanisha
mnyama mkali aliye tayari kurarua mtu muda
wowote.
Pamoja na sifa zote lakini hata mara moja
sikuwahi kukubaliana naye halafu akaenda
kinyume na makubaliano. Wakati wa
mazungumzo kutofautiana lazima, ila
makubaliano yakishafikiwa atatenda kama
ambavyo tuliafikiana.
Ni tofauti na wasanii wengi tu ambao
hawatumii ‘madude’ lakini si waaminifu katika
makubaliano hata kama yapo kwa maandishi.
Chidi akiwa jukwaani, anajua afanye nini kwa
wakati gani kwa kuangalia sura ya hadhira
ambayo anacheza nayo.
Mtazame Ray C, alilishika soko la Bongo Flava
siyo Tanzania tu, Afrika Mashariki kwa jumla.
Wakati huo dada yetu huyo alitambulika zaidi
kwa jina la ‘Kiuno Bila Mfupa’ kutokana na
uhodari wake wa kuzungusha nyonga yake,
japo kizembezembe, maana huwezi
kufananisha na vya wakata nyonga wa siku hizi
kama Snura na Shilole.
Wakati Ray C akiwa amelegea kwa matumizi ya
madawa ya kulevya, nilizungumza na mdau
mkubwa wa muziki Kenya, Refigah anayemiliki
lebo ya Grandpa Records, akanieleza
masikitiko yake kisha akaniambia: “Pamoja na
hali aliyonayo, Ray C akiwa Kenya ni biashara
kubwa, Wakenya wanampenda sana, pesa zake
zipo njenje.”
Mwanamuziki lulu barani Afrika, Brenda
Fassie, alifariki dunia dunia mwaka 2004.
Ripoti za kifo chake zipo wazi kwamba
kilichomsababishia mauti ni mdawa ya
kulevya, kwani asubuhi ya siku yake ya
mwisho, alitumia kiwango kikubwa cha
Cocaine.
Laiti kama Ray C angechukua kifo cha Brenda
kama shule kwake, sina shaka kwamba
pengine angekaa mbali na mihadarati. Tatizo ni
kwamba akili ya binadamu hufanya kazi
tofauti, mara nyingi hushawishika kufanya
yanayokatazwa. Reverse psychology ndiyo
sababu ya Hawa kumshawishi Adam kula tunda
la mti wa katikati kwenye Bustani ya Eden.
Mwanzoni mwa miaka ya 2000, mkongwe wa
Hip Hop Tanzania, Terry Msiagi ‘Fanani’ wa
Kundi la HBC, alishaanza kulalamika kwamba
matumizi ya madawa ya kulevya
yamempotezea dira na anatamani kuacha.
Yaani kadiri watu wanavyolalamika, ndivyo na
wengine wanavyoshawishika kutumia.
Mkongwe Mack 2B Simba hatunaye, kifo chake
kilifuata baada ya afya yake kuzorota
kutokana na matumizi ya madawa ya kulevya.
Mateso ya Banza Stone na hata kifo cha Ngwair
ni mifano hai, sasa ni kwa nini bado zipo
taarifa kwamba akina TID wanatumia unga?
Ulimwengu umeshapoteza vipaji vingi kupitia
madawa ya kulevya. Kuna ambao walikuwa
wanatengeneza fedha nyingi kwa vipaji vyao
kama Amy Winehouse, Whitney Houston,
Heath Ledger, Cory Monteith na wengineo, leo
hawapo nasi. Unga uliharakisha vifo vyao.
Kuna mastaa kama Lindsay Lohan, Robert
Downey Jr, Charlie Sheen, Chris Brown, Bobby
Brown, Britney Spears na wengineo wengi,
wamegeuka mateja. Maisha yao
yanavyoharibika si kificho lakini hawajifunzi.
Vipaji vinapotea, nafasi yao ya kutengeneza
pesa inakuwa finyu. Mashabiki hawapendi
mateja.
Ukitaka kuthibitisha hilo ni kuwa
mwanamuziki hata awe anapendwa vipi,
akisharipotiwa kutumia madawa ya kulevya,
hupoteza chati yake haraka sana. Ndiyo maana
leo hii ni kazi sana kuwarudisha sokoni wale
ambao jamii iliwatema kwa sababu ya uteja.
Watafanya muziki mzuri lakini mapokeo si
kama zamani.
Wakati muziki wa Tanzania ulikuwa huongei
kitu mbele ya Q Chiller, ikabainika kuwa
mwanamuziki huyo anatumia ‘madude’. Hapa
ifahamike kuwa unga husababisha ufanisi wa
kazi ushuke, kisha jamii humuona mhusika
kama mtu wa tofauti, maana mtumia madawa
ya kulevya ni mhalifu.
Sishangai mtu anapoibiwa vifaa vya gari lake
akimtaja Lord Eyez kwa sababu mwenyewe
aliamua kujipa sifa mbaya. Wapo wanamuziki
wakongwe wanakaa kimya na wakitoka
wanarudi na heshima zao kwa sababu
hawakuwahi kujiingiza huko. Hata kama
walijaribu, hawakutangazwa.
KWA NINI UNGA NA WASANII?
Nimeshafafanua kuwa wasanii hawajifunzi
licha ya kuwepo mifano mingi, sasa kwa nini
wanaendelea kujiingiza? Zipo sababu kadhaa
ambazo nitazifafanua moja baada ya nyingine
kutokana na uchunguzi ambao nimeufanya.
Kwanza; kundi kubwa la wanamauziki
wanajiingiza kwenye matumizi ya madawa ya
kulevya kwa sababu ya kuiga. Mtu anaweza
kumuona mwenzake anatumia, kwa fikra zake
akadhani ana faidi sana, hivyo naye kuamua
kujaribu. Wanaojaribu wengi huwa hawaachi,
mwisho wanatambulika kama mateja rasmi.
Niliwahi kuzungumza na Msafiri Diouf wa
Twanga Pepeta, akaniambia kuwa wakati Aisha
Madinda anataka kujiingiza kwenye unga,
alimuonya kwa sababu alishaona athari zake
lakini mwanadada huyo aliona anabaniwa, kwa
hiyo akaanza kubwia.
Pointi ya kuiga, hutokana na kuangalia hata
wasanii wa nje. Mathalan, mtu anamuona Chris
Brown, kisha anaona kwamba na yeye anaweza
‘kulanduka’. Hajui kama mwenzake ana pesa,
kwa hiyo anapata huduma nzuri kama chakula
na hata kusafisha damu, wa kwetu akijiingiza
tu, miezi miwili tayari ‘alosto’.
Nifafanue kuwa haina maana ukiwa na pesa
nyingi ndiyo ruhusa kutumia, la hasha!
Namaanisha kuwa akina Chris wanapata
huduma ambayo angalau inawafanya
wasichoke haraka. Ila kuchoka ni lazima ndiyo
maana ukipima muonekano wake kabla na
baada utaona tofauti kubwa.
Pili; wapo wanaingia kwenye uteja kwa sababu
ya makundi. Unakuwa na rafiki ambaye
anatumia lakini hujui, unamgongea sigara,
kumbe mwenzake ameichanganya na unga.
Ukivuta unalewa, unapata stimu, siku nyingine
unaulizia kama ile, mwisho nawe unakuwa
mtumiaji.
Niliwahi kumuuliza Maunda Zorro baada na
yeye kusikia anatumia, kwanza alinihakikishia
kwamba hatumii kabisa, ila akanipa ushuhuda
wa rafiki yake mmoja aliwahi kuonja ‘fegi’ ya
mwenzake studio ambayo ilikuwa
imechanganywa na madude.
Upo mfano wa mwanamuziki Kulwa wa
Mapacha Maujanja (alikuwa familia ya Vinega).
Yeye kwa kauli yake aliniambia kuwa aliwahi
kugongea sigara ya wasanii wenzake (alinitajia
majina yao) pale Maisha Club lakini
alichokutana nacho kilikuwa tofauti, alilewa na
siku iliyofuata aliumwa na kichwa vibaya
mpaka kujihisi anataka kurukwa na akili.
Tatu; ipo imani ya wasanii kwamba ukitumia
madawa ya kulevya unakuwa wa kileo zaidi na
hata sanaa utafanya kwa kiwango cha
kimataifa. Mwana Hip Hop anaamini akibwia
unga, basi atakuwa kama Snoop Dog, The
Game, Lil Wayne na wengineo wa Marekani.
Hivyo basi, mwanamuziki anaamua mpaka
kujidunga kwenye mishipa akiamini ndivyo
anavyokuza sanaa yake. Matokeo yake badala
ya kuwa msanii mkubwa, anageuka kuwa teja
wa kutupwa. Usicheze kabisa na madawa ya
kulevya.
Nne; msongo wa mawazo ni sababu nyingine.
Wapo wasanii soko linawakataa, pengine na
majukumu ya kifamilia yanawaandama.
Wakitazama kuna wenzao wanatengeneza
fedha kwa kasi kubwa kama ambavyo na wao
iliwahi kuwa upande wao.
Hali hiyo huwa inawachanganya vichwa
wasanii kiasi cha kuamua kujiingiza kwenye
matumizi ya madawa ya kulevya, wakiamini
wanatafuta suluhu ya msongo wa mawazo
wakati kumbe wanakwenda kujiharibia maisha
yao kwa jumla.
Tano; wapo wanaoingia kwa sababu ya tamaa,
mfano msanii anakubali kubebeshwa madawa
na kusafiri nayo kwenda nje kuuza. Hao
wanaitwa mapunda. Matokeo yake
wanajiingiza kwenye kutumia wakati
mwanzoni walijiapiza kusafirisha tu.
Kuna ambao waliamua kutumia baada ya
kuchanganyikiwa kutokana na kudhulumiwa
pesa za kusafirisha mzigo, wengine walitamani
tu kuonja ili wajue wanachokisafirisha kina
ladha gani. Ila yote kwa yote, mwisho ni uteja.
USHAURI
Wasanii wetu wanaweza kuepukana na
matumizi ya madawa ya kulevya kama tu
watazingatia kazi zao na kujiweka mbali na
mambo hayo ambayo nimeyataja kuwa sababu
ya wengi kujiingiza kwenye uteja.
Muhimu ni kuzingatia kwamba kazi yao ina
thamani kubwa, kwa hiyo wailinde. Na
watambue kuwa kuharibika kwao, husababisha
maumivu kwa mashabiki wao, maana kazi zao
huingia ndani ya mioyo ya mashabiki ambao
wakisikia habari zao mbaya, huumia sana na
kuvunjika mioyo.

author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Featured Posts

Recent Posts

About us

Popular Posts

Translate

Total Pageviews

Copyright © jaka classic | Designed By Code Nirvana